Historia ya Sayansi ya Tawhid


Mabadiliko ya mafunzo ya Tawhid yalianza kutokea baada ya Uislamu kusambaa na kutoka nje ya Bara Arabu, kuanzia Uajemi hadi Afrika ya Kaskazini, watu wa nchi hizi walipoingia kwenye Uislamu baadhi yao wakaanza kuandika na kujadili juu ya ufahamu wao wa kifalsafa wa dhana ya Mwenye Enzi Mungu, ndipo mchanganyiko ulipoanza kutokea na kusababisha hatari kubwa ya kupotea kwa mtazamo sahihi wa Tawhidullah.
Wakati wengine walifanya hivyo kwa kutokujua au kutoifahamu Tawhid wako ambao kwa nje waliukubali Uislamu hali lengo lao lilikuwa ni kuupiga vita nao waliona kuwa ni fursa nzuri ya kuichafua dini hii kwa kubomoa na kuvuruga ukweli juu ya Tawhid ya Allah (عز وجل). Hii ilitokana na ukweli kwamba kwa wakati ule walishindwa kuupiga vita Uislamu kwa silaha.
Kwa mujibu wa wana-historia mtu wa mwanzo kuuathiri Uislamu juu ya dhana kwamba hakuna Qadara ya Allah (Azza Wa Jalla) alikuwa Sausan ambaye alisilimu kutoka kwenye Ukiristo. Sausan baada ya kuathiri sehemu ya Umma juu ya falsafa zake alirtadi kwa kurejea kwenye Ukiristo. Hata baada ya Kuritadi kwake mfunzo yake potofu yaliendelezwa. Kwa mfano mwanafunzi wake Ma’bad ibn Khalid Al Juhani Al Basrawi aliendeleza mafunzo ya Sausan hadi alipokuja kukamatwa na kuhukumiwa kifo mwaka 700 CE wakati wa Khilafa ya Umayya.
Kufa kwa Ma’abad hakukuwa mwisho wa mafunzo haya potofu katika jina la Uislamu. Mmoja kati ya wanafunzi Ma’abad, Ghailan ibn Muslim aliyaendeleza mafunzo hayo. Hatimaye naye akakamatwa na kuhukumiwa kifo wakati wa utawala wa Hisham ibn Abdul Malik (724 – 743 CE)
Mafunzo haya ya kutoamini Qadara ya Allah (عز وجل), na hivyo kuwepo kwa dhati (free-will) tu yaliendelea kusambaa na kutanuka na kupata wafuasi wengi zaidi.
Al Ja’ad ibn Dirham sio tu aliunga mkono na kufundisha falsafa hizi bali pia alijaribu kuupanua upotofu huo kwa kuingiza falsafa za Aristotle na Plato katika kumfahamu Mwenye Enzi Mungu. Haya yalikuwa ni mafunzo wa Ukiristo. Al Ja’ad alijaribu kuzifasiri upya aya za Qur’ani zinazozungumzia Tawhid na kutoa maana inayokubaliana na mafunzo yake potofu. Al Ja’ad naye baada ya kufundisha upotofu hadi kufikia kuzikataa baadhi ya sifa za Allah (عز وجل) kama vile kuona kusikia na kadhalika, alihukumiwa kifo wakati wa utawala wa Khalid ibn Abdallah (736 CE) kwenye khilafa ya Umayya.
Baada ya wimbi hili la upotofu kuwa kubwa kwa wafuasi na kwa upana wa mafunzo, maulamaa wakaona kuna umuhimu wa kupigana nalo kielimu badala ya kusubiri watu kama hawa wakamatwe na kuhukumiwa. Kazi hii ya kupinga mafunzo potofu na kuhakikisha tawhid ya Allah inafahamika kwa mujibu wa Qur’ani na mafunzo ya Mtume (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) haikuwa rahisi, kwani kabla hapo ya tawhid haikufundishwa kama somo. Mapambano yaha ndiyo yaliyozaa Sayansi ya Tawhid na mgawanyiko wa ar Rubuubiya, al Uluuhiya na al Asmaa wa Sifaat.
Kwa hiyo ni lazima tufahamu kwamba lengo la mabadiliko haya nalo ilikuwa ni juhudi ya kunusuru elimu hii muhimu juu wa ukweli wa namna tunavyotakiwa kumfahamu Allah (عز وجل). Leo Waislamu hatuna budi kumshukuru Allah (عز وجل) na kuzithamini juhudi za Maulamaa hawa kwamba hatufunzwi Tawhid kama alivyotaka Aristotle na Plato.