Adabu za Kusoma Qur'ani

Adabu za usomaji wa Qur’ani tukufu zimegawika makundi mawili, Adabu za ndani ya nafsi ya msomaji au adabu za moyo na mambo ambayo msomaji anatakiwa kuyatimiza kabla au wakati wa kusoma Qur’an tukufu.
Adabu za Moyoni (Nafsi)
Nia au Ikhlaas
Msomaji wa Qur’ani hana budi kuwa na nia sahihi anapokusudia kusoma Qur’an tukufu. Nia ni msingi mkubwa wa dini hii kwa vile huwa ni tofauti baina ya kukubaliwa au kukataliwa kwa amali au ibada na Allaah ta'ala. Nia sahihi ni kusoma au kujifunza Qur’ani kama ibada kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah ‘azza wa jall. 
Amiril Mu’minin, Abu Hafs, Umar ibn al Khattwab radhi Allahu ‘anhu amesimulia kwamba amemsikia Mtume Salla Llahu ‘alayhi wa sallam akisema:
إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّمَا لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى...
Matendo (amali) hutokana na nia na kila mmoja atalipwa kutokana na nia...
Ni muhimu kuepuka kuwa na nia zilizokuwa si sahihi tunapotaka kusoma Qur’an. Nia kama hizi mtu huwa nazo kuwa makusudi au wakati mwingne bila ya kuwa na mwamko nazo. Mfano kusoma ili kuwapendezesha wasikilizaji au ma-amuma katika swalaah, au ili kuonekana kwamba wewe ni mahiri mno katika kusoma Qur’ani, nia kama hizi hupelekea mtu kufanya riyaa (kujionesha kwa watu) na hili ni kosa au dhambi katika Uislamu.
Kumtukuza Aliyeiteremsha
Tunaposoma Qur’ani ni muhimu kuwa katika hali ya kumkumbuka Allah ‘azza wa jall. Pia ni vyema kuwa na mwamko kwenye nafsi zetu ya kuwa Allah ni mwenye kutushuhudia tunaposomwa Qur’ani. Jaribu kuvuta fikra ni kiwango gani cha adabu, unyenyekevu, heshima na utiifu tunatakiwa kuwa nacho wakati aliyetuumba anatusikiliza. Allah anasema katika Qurani tukufu, surati Yunus:
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِنْ قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ...
Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo...
'Ibra (Mazingatio)
Ni muhimu sana kuzingatia kwamba Qur’ani ni maneno ya Allah yenye lengo la kutupa mwongozo ambao ndio msingi wa mafanikio Duniani na Akhera. Allah ta’ala  amesema katika kitabu chake hichi kitukufu katika Suratis Swaad:
كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ
Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili (38:29)
Hivyo basi aya hii inabainisha wazi kwamba wajibu wetu ni kufanya mazingatio ili tuwaidhike au tunasihike.
Khushu'u
Mbali na kuzingatia, kusoma au kujifunza kusoma Qur’ani ni ibada. Hivyo basi moja katika mambo muhimu ni kufanya unyenyekevu, isiwe tunasoma Qur’ani haifiki hata kooni. Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam pamoja Masahaba (Mwenyezi Mungu awawie radhi) walikuwa wakitokwa na machozi, wakiingiwa na khofu, wakipata  tamaa ya malipo ya Allah ta'ala na kadhalika kutokana na aya za Qur’ani.
Akili na moyo ni lazima viwepo msomaji anapoisoma Qur’ani. Tuwache tabia ya kufikiria mambo mengine tunaposoma Qur’ani kwani kama tulivyosema kwamba kusoma Qur’ani ni ibada. Kuwa na mawazo mengine kunapelekea msomaji kutozingatia anachokisoma. Ni vyema tuwe tunamkumbuka aliyetuletea ujumbe yaani Allah ‘azza wa jall na tuwe tunazingatia ujumbe wenyewe. Allah ‘azza wa jall ametuambia katika Qur’ani:-
وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنْصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ 
Na isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemewa (7:204)
Allah ta’ala anatuambia msikilizaji tu anatakiwa anyamaze ili apate kurehemewa, bila shaka msomaji anatakiwa kuwa na utulivu na unyenyekevu zaidi.
Kubinafsisha Ujumbe wa Qur’ani
Tunaposoma Qur’ani tujitahidi kuzisemesha nafsi zetu kwamba huu ni ujumbe unaonihusu mimi, yaani kama ni katazo basii msomaji ndiye anayekatazwa na kama ni amri basi msomaji ndiye anayeamrishwa. Hii kwa uwezo wa Allah huenda ukatupa matumaini juu ya mema yetu na kutupa khofu juu ya yale ambayo Allah sub-hanahu wa ta’ala ametukataza.
Adabu nyinginezo
Mbali na adabu za moyo kuna mambo ambayo tunahitaji kuyafanya au kuyatimiza tunaposoma au kabla ya kusoma Qur’ani kama ifutavyo:-
Twahara
Twahara katika mwili, nguo na mahala tunaposomea, unapokuwa ni mwenye kuushika msahafu basi ni lazima kuwa na udhu, na ikiwa unasoma kutokana na kumbukumbu (kwa ambaye amehifadhi Qur’ani) basi halazimiki mtu kuwa na udhu lakini awe ametoharika kutokana na janaba, hedhi au nifasi.
Kibla
Japokuwa hii si nguzo lakini ni vyema kwa msomaji wa Qur’ani tukufu kuelekea kibla, na hasa kutokana na uwezekano wa kuleta sijdat at tilaawa (sijda ya kusoma Qur’ani)
Kusoma kwa kukata kata
Tujitahidi kuepuka kukatisha kusoma Qur’ani katikati na kufanya mambo mengine kama mazungumzo na kadhalika na pia tusiwe ni wenye kuwakera watu walioko karibu yetu, kwa mfano kusoma Qur’ani msikitini kwa sauti kubwa hali ya kuwa kuna mtu karibu yako anaswali.
Sijdat at Tilaawa
Kusujudu katika aya ambazo Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam amesujudu. Aya hizi kwa idadi katika Qur’ani ni kumi na nne, sijda hii hujulikana kama Sijat At Tilaawa (yaani sijda ya kisomo) Mfano Aya ya mwisho ya suratul ‘Alaq:
كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِبْ [٩٦:١٩]
Isti’adha
Tuanze kwa kumuomba Allah sub-hanahu wa ta’ala atulinde na hila za shetani kwa kusema:
اَعُوْذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيطنِ الرَّجِيْم
Tufanye hili kwa sababu Allah ‘azza wa jall anatuambia katika Qur’ani tukufu:
فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ [١٦:٩٨]
Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni
Basmallah
Bismillahi, yaahi kuanza kwa jina la Allah kila tunapoanza kusoma au tunapoanza sura yoyote kwa kusema: 
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.
Katika surat Al Fat-ha hii ni aya, yaani ni sehemu ya sura hii. Katika Surat Al Baraa huwa haisomwi Baslamallah, sababu ni kwamba Mtume Salla Llahu ‘alayhi wa sallam hakusoma Bismillahi mwanzoni mwa sura hii ambayo pia hujulikana kama Surat At Tawba.
Kusoma Dua
Kuitikia aya ambazo Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam amezijibu au kuziitikia au kuomba du’a. Kwa mfano katika aya ya mwanzo ya suratul Ghaashiyyah isemayo:
ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُمْ [٨٨:٢٦]
Msomaji ataomba kwa kusema: 
اللَّهُمَّ حَسِبْنِي حِسَابً يَسِيْرَا