Maana na kanuni za Ahkami tajwid

Maana ya Ahkami tajwid

Tajwid katika lugha maana yake ni kuboresha, tajwid inatokana na neno jawwada. Tajwid kama somo au sayansi ya Qur’ani hujumuisha mambo matatu yafuatayo:-
إِخْرَاجُ كُلِّ حَرْف مِنْ مَخْرَخِهِ
Kutamka kila herufi (kwa usahihi) kutoka katika sehemu yake ya kumtakia: Kila herufi huwa na sehemu yake maalum ya kutamkia kwa mfano herufi ya baa (ب) hutamkwa kwa kukutanisha midomo miwili au ‘ayn (ع) ni herufi ya katikati ya koo.
حَقُّ الحَرْف
Haki ya herufi: yaani kuipa haki kila herufi katika usomaji, haki za herufi ni sifa za kudumu ambazo daima humabatana na herufi.
مُسْتَحَقُّ الحَرْف
Mustahaq ya herufi: hizi ni sifa za herufi ambazo sio za kudumu, yaani wakati mwingine huwepo na baadhi ya wakati huwa hazipo, kwa mfano Idghaam.
Faida kubwa inayopatikana katika somo hili ni kuepuka kusoma Qur’ani bila ya usahihi na hivyo kupelekea msomaji kusoma Qur’ani kwa namna inavyotakiwa. Makusudio hasa ni kwamba Qur’ani isomwe namna alivyosomeshwa Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam na malaika Jibril ‘alayhis salaam.
Hukumu ya Kusoma kwa Tajwid
Kuwa na elimu ya tajwid ni fardhi kifaya (فَرْض كِفَا يَة) fardhi yenye kutoshelezeana kwa maana ya kwamba iwapo yupo mwenye elimu ya tajwid katika jamii huitosheleza jamii nzima. Ama kuhusu kutumia au kutekeleza tajwid katika kusoma ni fardh ‘ain (فَرْض عَيْن) yaani ni wajibu wa kila msomaji asome kwa kufuata hukumu zote za tajwid.