Tawhid ar Rubuubiya

Tawhid ar Rubuubiya inalenga kumpwekesha Allah sub-hanahu wa ta’ala katika kazi ya ‘uungu’ au ‘umola’, katika hili hana mshirika wala msaidizi. Allah ‘azza wa jall pekee ndiye aliyeumba kila kitu tangu kabla ya kuwepo chochote. Ameumba na kudumisha alivyoviumba hali ya kwamba havihitajii.  Ni Mola, mlezi na mwenye kudumisha, ni Mola pekee wa mbinguni na ardhini na vilivyomo baina yake na hata nje yake.
Asili ya neno Rubuubiya ni Rabb. Kwa lugha ya Kiswahili tunalifasiri Mola au Bwana, yote ni sawa kwa vile Mola lina asili ya neno la kiarabu Mawla, yaani bwana. Sifa za Mola ni mbili nazo ni mlezi na muumbaji. Ni lazima tuwe na yakini kwamba yakuna kinachoweza kutokea au kubadilika katika maumbile (kuumbika) bila ya matakwa ya Allah ta’ala.
Misingi na asili ya dhana ya Tawhid ar Rubuubiya inapatikana katika aya mbali mbali za Qur’ani. Allah (Azza  wa Jalla) anasema:
وَاللَّهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ
Na hali Allah ndiye aliyekuumbeni nyinyi na mnavyovifanya (37:96)
اللَّهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ
Allah ndiye Muumba wa kila kitu na yeye ndiye Mlinzi wa kila kitu (39:62)
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّهِ يَهْدِ قَلْبَهُ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
Haukufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Allah, na anayemuamini Allah huuongoza moyo wake. Na Allah ni mjuzi wa kila kitu (64:11)
Ufafanuzi wa aya:
Na hali Allah ndiye aliyekuumbeni nyinyi na mnavyovifanya: Aya hii inatosha kwetu sisi binaadamu kuondokana na kiburi na dhana potofu kwamba sisi ni viumbe wenye elimu ya kiwango cha juu sana. Dhana hii hupelekea baadhi ya wasioamini kuwafanya kuwa ni kigezo cha kutokuwepo kwa Mungu. 
“Haukufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Allah” Allah ‘azza wa jall ndiye aliyeumba uhai na umauti, na vile vile misiba ya aina yote, kwa hiyo kila jambo linatokea kwa idhini ya Allah ta’ala na hakuna ambalo linaweza kutokea kinyume na vile ambavyo Allah subhanahu wa ta’ala amepanga tangu kabla jambo hio halijatokea.
“na anayemuamini Allah huuongoza moyo wake”  Aya hii tunajifunza kwamba ili tupate hidaya (muongozo) ni lazima kwanza tuamini. Hidaya ni jambo ambalo sisi wanaadamu tunalihitajia mno na halimo mikononi mwetu, Allah ‘azza wa jall amejaalia kwamba sisi tuwe ni wenye kuomba hidaya kuliko jambo lingine lolote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila tunaposali humuomba Allah ‘azza wa jall hidaya kwa mujibu wa idadi ya rakaa kwa kusema katika Surat Al Fat-ha:
اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ
Tuongoe katika njia iliyo nyooka
Allah ni Mjuzi wa kila kitu: huu ni ujumbe mzito kwa wasioamini kuwepo kwa Allah ta’ala eti kwa kuwa hakuna ushahidi wa kisayansi juu ya kuwepo kwake (Atheism), hii inatokana na fikra na nadharia potofu kwamba katika Ulimwengu tulio nao wapo (na hasa hawa “ma-atheist”) wanaodhani maendeleo ya kisayansi na teknolojia ni ya kiwango cha juu, na kwamba mwanadamu ana elimu ya kiwango cha juu mno. Watu hawa wanatakiwa wakumbuke kwamba hawana ujuzi hata kidogo juu wa roho hata ya kiumbe mdogo au dhaifu kuliko vyote, hii inadhirisha uchache wa elimu ambayo Allah sub-hanahu wa ta’ala ametupa. Kwa hakika elimu ya Allah ‘azza wa jall ni timilifu kwa namna zote.
Aya hizi zinatosha kutoa dalili juu wa Tawhid ar Rubuubiya. Sio tu aya hizi zinaelezea kwamba Allah ndiye muumba bali pia zinatoa maelezo kama vile yeye ndiye mlinzi wa kila kitu na muendeshaji wa matendo yetu na mambo yote. Hata  misiba inayotukuta nayo pia ni kwa idhini ya Allah (ta’ala). Kwa hiyo hakuna shaka yoyote kwamba Tawhid ar Rubuubiya ni mafunzo ya Qur’ani tukufu.