FIQ-HI YA TWAHARA - UTANGULIZI


Shukrani zote zina mstahiki Allaah, Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume wa Allaah na watu wake na sahaba zake, pamoja na wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyamah.
Uislamu ni dini ya kujitoharisha; ni  dini yenye kusisitiza mno kwenye suala la usafi, usafi wa moyo na hata usafi wa nje; yaani mwili na mazingira. Dini hii imetoa ufafanuzi wa hali ya juu kuhusu mambo yote tunayoyahitaji katika suala la twahara,  Uislamu umeweka wazi juu ya kanuni zote  ambazo zinamnufaisha mwanadamu katika maisha yake, hakuna ambacho ni chenye manufaa katika maisha na Uislamu umekiacha, twahara ni moja katika ya mambo yenye manufaa makubwa kwa mwanadamu ndio maana Uislamu ukasisitiza utekelezaji wake.

Kuna ibada ambazo katika Uislamu haturuhusiwi kuzitekeleza mpaka tuwe katika hali ya twahara. Hii inatokana na ukubwa na umuhimu wa ibada hizo. Mfano wa ibada hizo ni Swalaah.
Swalaah ni nguzi ya pili ya kiislam baada ya shahada, swalaah ndiyo inayotofautisha baina ya Muislamu na Kaafir. 

Jaabir bin ‘Abdullah (radhi za Allah zimshukie) amesema: Nimemsikia Mtume salla Llahu ‘alayhi wa sallam akisema: “Baina ya mtu na kaafir au kufuru ni kuacha swalaah” [Sahih Muslim Vol. 1, Hadith 247, uk 170-171]
Swalaah ni nguzo muhimu mno katika Uislamu, ni jambo la mwanzo tutakalo ulizwa siku ya Qiyamah. Anasimulia Abu Hurayrah (radhi za Allah zimshukie) kwamba Mtume (rehma na amani juu yake) amesema “Kitu cha mwanzo kitakacho hesabiwa siku ya Qiyamah ni Swalaah...” [Sunnan an Nisaa vol 1, Mlango wa 5, Hadithi ya 467]
Swalaah haipokelewi wala haiwi sahihi mpaka anayeswali awe na twahara.  Jaabir ibn ‘Abdallah (radhi za Allaah zimshukie) anasimulia kwamba Mtume wa Allaah (rehma na amani juu yake amesema “Ufunguo wa Pepo ni Swalaah na Ufunguo wa Swalaah hi udhu” [Sunan ibn Majaah Vol 1, Mlango 1, Hadith 4] [Abu Twahir Zubair ‘Ali Za’i amesema hadithi hii ni Hassan]
Inshallah katika makala zijazo tutazungumzia fiqh ya twahara kwa mujibu wa Qur’aan na sunnah iliyosahihi ya Mtume Muhammad rehma na amani juu yake.