MAZINGATIO KATIKA HIJRAH YA MTUME (rehma na amani juu yake)


Bila shaka wengi wetu tumesoma au kusikia kuhusiana na Hijra(kuhama) ya mtume kutoka Makka na kuelekea Madina. Hapa ndipo ilipo anza tarehe ya kiislamu. Katika safari hii ya mtume kuna mazingatio mengi sana, leo hii tutazungumzia baadhi ya haya mazingatio:

1: Mazingatio ya uhamaji:
Mwenyezi Mungu alitoa idhini kwa Mtume wake na  Waumini kuhama toka Makkah kutokana na madhara mbali mbali waliyo kuwa wakiyapata kutoka kwa makafiri wa Kiquraysh. Katika haya madhara ilikuwa ni kuwazuia waislamu kuisimamisha dini yao, wakateswa na kuadhibiwa vikali.

Ndio Allah alipo toa ruksa hii kwa mtume na masahaba wake ili waweze elekea sehemu watakayokuwa na uhuru wa kumuabudu Allah na kusimamisha uislamu pasina ya bughudha zozote.
Maana ya kuhama kisheria haiishii katika kutoka sehemu moja na kuelekea sehemu nyingine, kutoka katika mji mmoja na kuelekea katika mji mwingine. Bali ni kulihama kila lile lililo katazwa na Mwenyezi Mungu ili mja maisha yake yote Yawe ni kwa ajili ya Allah.
Kuyahama madhambi na maasi, kuyahama matamaniyo yenye kumpeleka mja kumuasi Allah, kuzihama sehemu zile unapofanyikia uovu kama vile madanguro, baa, vilabu na mengineyo.
Kuhama kutoka katika ufinyo wa Dunia na kuelekea katika upana wa akhera, hali itakayo mpelekea mja aishi hali ya kujua ya kwamba hapa duniani sio ndio mwisho wa maisha bali kesho akhera kuna maisha ya milele na milele.
2: Subira na yakini ni njia ya kunusuriwa na kumakinishwa:
Baada ya miaka 13 ya kubanwa, kuteswa, kunyanyaswa na kudhulumiwa, muda ambao alio uishi mtume na maswahaba kule Makka,Allah akawaandalia waislamu Ardhi nzuri na kuingiza imani katika nyoyo za Maanswari na kuanza mlolongo wa nusra na kumakinishwa (kuthibitishwa) katika ardhi kwa wale watu walio kuwa na subira na yakini yaani mtume na maswahaba zake.
قال الله تعالي:
إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi [Surat Ghafir:51]
Hakika njia ya kushikamana na dini ya Allah na kuwalingania  watu juu ya dini hii ya kweli,ni njia iliyo zungukwa na mitihani mbali mbali na mambo ya kuchukiza
Na baadhi ya nyakati huwa ni mambo yenye kukatisha tama.
Lakini kwa mwenye kusubiri na kuthibiti basi huyo ndiye atakaye faulu kuneemeka na kupata furaha ya kweli ya maisha.
(والله غالب على أمره ولكن أكثر الناس لا يعلمون)
سورة يوس:ف21
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
(Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui) Surat Yusuf:21
3: Mazingatio ya kumtegemea Allah na kushikamana na kamba (dini) yake:
Kwa hakika safari ya kuhama kwa mtume ilikuwa ni safari iliyo zungukwa na hatari na hata tishio la umauti. Kwani makafiri baada ya kusikia habari za kuhama kwa mtume [rehema na amani ziwe juu yake] waliizunguka nyumba ya mtume wakiwa na mapanga na silaha nyingine wakiwa na nia ya kumuua, kwa hiyo wao walikuwa wakisubiri atakapo toka tu basi wammalize. Lakini kwa uwezo wake Allah [taa’ala] alimsalimisha Mtume wake na kumtoa salama pasina ya makafiri kumuona.
Na pindi alipo ondoka nyumbani kwake na kwenda kujificha pangoni, makafiri wamefika mpaka katika mlango wa pango kiasi kwamba mmoja wao akiangalia chini tuu basi atamuona mtume na Abubakr (radhi za Allah zimshukie) lakini Allah ta’ala akawanusuru mtume na Abubakr.
Vilevile Suraka alipokuwa akimfukuza Mtume (rehma na amani juu yake) mpaka akawa kamkaribia kabisa akawa akisikia kisomo cha mMume, lakini ghafla miguu ya farasi wa Suraka inadidimia chini tena ni sehemu ya mawe! Kisha baada ya hapo linatimuka vumbi kali na kumfanya Suraka asimuone Mtume (rehma na amani juu yake).
Mtume (rehma na amani juu yake) katika hali zote hizi alikuwa ni mwenye kuthibiti na kumtegemea Allah ‘azza wa jall na kuwa na yakini Naye.
Kwani yeye anajua kwa yakini kwamba maadamu Allah ta’ala kaniahidi nusra basi ataninusuru tu.
Hivi ndivyo inavyo kuwa hali ya muumini, vyovyote vile yatakapo mzidia matatizo na mitihani basi hatetereki kwani yeye ajua ahadi ya Allah sub-hanahu wata’ala  mbele ya mawalii wake (waja wenye kumuamini Allah na kumtii), na anajua ya kwamba baada ya dhiki ni faraja.
قال الله تعالي:
( فإن مع العسر يسري .إن مع العسر يسرا) سورة الشرح : 5-6
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
(Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi. Hakika pamoja na uzito upo wepesi) Surat Asharh:5-6
Allah kasema hakika pamoja na uzito upo wepesi licha ya kwamba kimoja hukitangulia kingine, yaani unaweza kuanza uzito kisha ukaja wepesi, lakini Allah kasema pamoja na uzito upo wepesi kuashiria ya kwamba penye uzito pasi wepesi huja haraka sana mpaka viwili hivyo vikafanywa kama vipo pamoja.
Kwa hiyo mja pindi utapopatwa na uzito juu ya suala fulani la kheri basi usikate tama bali azidi kuchukua sababu na kusubiri faraja ya Allah ambayo ipo karibu naye.
4: Mazingatio juu ya miujiza ya Allah:
Je mshawahi kumuona mtu dhaifu aliye zungukwa na maadui wenye silaha kali, kisha mtu huyu dhaifu anatoka na kuwamwagia  maadui mchanga nyusoni mwao na hawamuoni?
Je mshawahi muona buibui anatanda utando wake katika mlango wa pango kwa muda wa saa chache tu?
Je mshawahi ona maadui wanamtafuta adui yao na kupanda mpaka mlimani na kusimama katika mlango wa pango pasina ya hata mmoja wao kujaribu kuangalia kilichomo katika pango?
Je mshawahi muona farasi akikimbia katika ardhi ngumu kisha miguu yake yadidimia kama vile anatembea katika tope? na kutimuka vumbi kali mpaka mbele kukawa hakuonekani?
Je mshawahi muona mbuzi mdogo ambaye hajazaa yakibubujika toka katika kiwele chake maziwa ya kutosheleza idadi ya watu wengi?
Hakika miujiza hii ni dalili tosha juu ya uwezo wa Allah, Na iwapo kama Allah atataka kuwanusuru waumini basi mizani yote hugeuzwa na mambo kwenda tofauti na inavyo fahamika kwa watu.
قال الله تعالي(إنما أمره إذا أراد شيئاً أن يقول له كن فيكون)
سورة يس:82
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
(Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa ) Surat Yaasin:82
5: Mazingatio katika Mapenzi:
Anasema Mtume (rehema na amani ziwe juu yake)
(لا يؤمن أحدكم حتى أكون أحب إليه من ولده ووالده والناس أجمعين)
(Hato amini mmoja wenu mpaka anipende kulikoni mtoto wake na mzazi wake na watu wote kwa ujumla) 
Mja hawezi kuwa mkamilifu wa imani mmpaka ampende mtume kulikoni watoto zake na wazazi wake. Mapenzi haya ndiyo yaliyo mfanya Abubakr (radhi za Allah ziwe juu yake) alie kutokana na furaha kwa kuungana na Mtume (rehma na amani juu yake) katika safari hii. 
Mapenzi haya ndiyo yaliyo mpelekea Abubakr avumilie maumivu ya kugongwa na nyoka pasina ya kutikisika kwa kuwa Mtume kalala juu ya mguu wake, pale walipo kuwa pangoni.
Mapenzi haya ndio yaliyo pelekea Abubakari kutoa mali yake yote kwa ajili ya Mtume na Uislamu kulikoni kutoa katika  nafsi yake na familia yake.
Mapenzi haya ndiyo yaliyo wafanya Maanswaari wakawa wakitoka nje ya Madina kila siku kipindi cha joto na jua kali wakimsubiri Mtume huenda akatokea.
Tupo wapi tunaodai kumpenda Mtume hali ya kuwa tukiasi mafundisho ya Allah aliyokuja nayo usiku na mchana na kujiweka mbali na suna zake?
6: Mazingatio katika kujitolea na kujitoa muhanga.
Hakika katuachia Mtume na maswahaba wake kurasa zenye kung`ara juu ya masuala ya kujitolea, sawa iwe ni kujitolea mali au hata nafsi kwa ajili ya kuinusuru dini hii tukufu. Walihama kwa ajili ya Allah pasina ya kujitetea ya kwamba wana watoto wadogo au hawana mali za kuwatosheleza au visingizio vingine. Kwani dunia ilikuwa haina thamani yoyote kwao wao ukilinganisha na Amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (rehma na amani ziwe juu yake)
Tukumbuke pindi Ally (radhi za Allah ziwe juu yake) alipolala katika kitanda cha Mtume na kujifunika, hali ya kuwa anajua ya kwamba makafiri wa Kiquraysh wapo nje na mapanga na huenda muda wowote wakaingia na kumpiga mapanga aliye lala katika kitanda kile, kwani kitanda kile kilikuwa ni cha Mtume (salla Llahu alayhi wasallam).
Na tukumbuke pindi familia ya Abubakr walipo kuwa wakiwafanyia Mtume na Abubakr huduma mbali mbali pindi walipokuwa pangoni, bila shaka walikuwa wakijua ya kwamba iwapo kama watagundulika basi huenda wakauwawa na makafiri ,lakini hata hivyo  hawakujali.
Hivi ndivyo walivyokuwa vijana wa maswahaba, tupo wapi vijana wa leo na kujitolea huku na kushikamana na  na kujivunia Uislamu? Baadhi yetu hata kutekeleza ibada ya swala tu imekuwa ni shughuli ngumu, je tutaweza kujitolea nafsi zetu???
Bila shaka vijana wenzangu kuna haja ya kuzinduka na kubadilisha mwelekeo, tunako elekea siko!
7: Mazingatio juu ya uelevu mbinu na kuchukua sababu.
Alikuwa Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) ni mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, mwenye yakini juu ya nusura yake na mwenye kujua ya kwamba Allah ta’ala ni mwenye kumtosheleza.
Lakini licha ya hayo yote mtume hakuwa ni mtu mwenye kupuuzia na mwenye kufanya mambo kienyeji enyeji. Bali Mtume aliandaa mbinu zilizokuwa ni madhubuti kisha akazitekeleza kwa hali ya usiri wa hali ya juu na umakini.
Kiongozi wa msafara: Muhammad sallaLlahu ‘alayhi wasallam
Msaidizi: Abubakr (radhi za Allah zimshukie)
Mtu wa kujitolea muhanga: Alliy (radhi za Allah zimshukie)
Masuala ya chakula: Asmaa bint Abibakr (radhi za Allah zimshukie)
Masuala ya habari: Abdallahi bin Abibakr (radhi za Allah zimshukie)
Kuwapoteza maadui: Aamir (radhi za Allah zimshukie)
Mtaalamu wa njia: Abdullah bin Ariikat (radhi za Allah zimshukie)
Sehemu ya kukaa kwa muda: Pango la Thawri.
Muda wa kuondoka: Baada ya siku tatu.
Njia ya kupitia: Kando kando ya bahari.
Yote haya ni dalili juu ya  werevu, mbinu na hekima za Mtume. Na ndani yake wito kwa umma wa Kiislam juu ya kupangilia mambo yao, kuyafanya kwa umakini na kuandaa sababu za kufanikisha jambo licha ya kumtegemea Allah
Mpitishaji wa sababu mwanzo na mwisho.
8: Mazingatio juu ya Ikhlas.
 Alikuwa Abubakr (radhi za Allah ziwe juu yake) akitoa mali zake kwa Mtume (rehma na amani juu yake) na katika ulinganiajia wa dini ya Allah na katika majukumu mbali mbali ya uislamu.
قال  الله تعالي(الذي يؤتي ماله يتزكى )سورة الليل:18
Anasema Allah mtukufu kwa kumsifu Abubakar:
(Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa)
Surat Allayli:18
Na katika safari hii Abubakari aliandaa vipandwa kwa gharama zake lakini mtume akamkatalia na kumrudishia thamani yake.
9: Mazingatio juu ya tarehe ya kiislamu:
Waisalamu kuwa na terehe yao ni sehemu miongoni mwa sehemu za utukufu  wa waislamu na kutofautiana mila nyingine.
Asili ya kuanzishwa kwa tarehe ya kiislamu ni kipindi cha Umar (radhi za Allah ziwe juu yake). ‘Umar alipata fikra hii ya Waislamu kuwa na tarehe yao itakayo kuwa ikitofautiana na watu wengine. Akawataka ushauri maswahaba je tarehe hii ianzie wapi?
Je tokea kuzaliwa kwa mtume? Au baada ya kupewa utume? au baada ya kuhama? Au baada ya kufariki?
Wakaafikiana ya kwamba tarehe ya kuhama ndilo  chaguo munasibu. Kwani kuzaliwa kwake mtume na muda wa kutumwa kwake ni masuala ambayo wanazuoni wametofautiana.
Ama muda wa kufariki kwake bila shake suala hili litapelekea huzuni, kwani hakuna msiba mkubwa zaidi ya kufiwa na Mtume (rehma na amani ziwe juu yake).
Kwahiyo Allah akawaongoza maswahaba juu ya kuchagua tarehe hii ya kuhama kwa Mtume.
Na waislamu wakashikamana nayo karne baada ya karne mpaka kufika muda huu ambao waislamu tumekuwa hatuzingatii tarehe yatu wala kuitilia umuhimu.Baadhi yetu tumekuwa hatuikumbuki tarehe hii isipokuwa mwezi wa Ramadhan au miezi ya Hijja.
Twamuomba Allah aturudishe katika dini yake na atutengenezee mambo yetu ,kwani Yeye juu ya kila jambo ni Muweza.