FADHILA ZA KUSALI RAKAA NNE KABLA NA BAADA YA ADHUHURI

Shukrani zote zinamstahiki Allah Mola Mlezi wa viumbe wote. Rehma na amani zimshukie Mtume pamoja na ali zake, masahaba wake na wale wote wenye kufuata mwenendo wake mpaka siku ya qiyama.

Miongoni mwa sunna muhimu ni sunna ya kusali rakaa nne kabla na baada ya sala ya adhuhuri. Hadithi ifuatayo inaeleza wazi juu ya fadhila za kusali rakaa hizo za sunna: 

عَنْ أُمِّ حَبِيبَةَ رضي الله عنها عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ( مَنْ صَلَّى أَرْبَعًا قَبْلَ الظُّهْرِ وَأَرْبَعًا بَعْدَهَا لَمْ تَمَسَّهُ النَّارُ ) ]روى النسائي (1817) والترمذي (428)]
Amesimulia Umm Habibah (رضي الله عنه) kuwa Mtume rehma na amani juu yake amesema: mwenye kusali rakaa nne kabla ya adhuhuri na nne baada yake moto hautomgusa. [An-Nasaa’i (1817) and at-Tirmidhi (428)]

 ولفظ الترمذي : ( مَنْ حَافَظَ عَلَى أَرْبَعِ رَكَعَاتٍ قَبْلَ الظُّهْرِ وَأَرْبَعٍ بَعْدَهَا حَرَّمَهُ اللَّهُ عَلَى النَّارِ)
Na katika riwaya ya at-Tirmidhi amesema: (mwenye kuzihifadhi rakaa nne kabla ya adhuhuri na rakaa nne baada yake Allaah atamharamishia moto) 

والحديث صححه الألباني في صحيح النسائي .
Hadithi hii imesahihishwa na Imam Albani katika sahihi an-Nisaa’i

Kuhifadhi hapa ina maana ya kuwa mwenye kuziendeleza au mwenye kudumu kwenye rakaa nne nne hizi, huku akiwa ni mwenye kuyafuata masharti na kila lile ambalo limeambatana na ibada ya sala. 

Rakaa nne hizi ni za kawaida ambazo tunazifahamu maarufu kama Kabliyya na Baadiyya ambazo wengi husali rakaa mbili mbili badala ya nne nne. Hata hivyo si makosa kusali mbili kabla na baada lakini fadhila hizi zimeelezewa kwa wale wenye kusali rakaa nne nne. Hivyo iwapo mja atasali rakaa mbili basi Allah atamlipa malipo mazuri.

Nyakati za rakaa hizi, zile za kabla husaliwa baada ya adhana ya adhuhuri (au baada ya kuingia wakati wa adhuhuri) na kabla ya kusaliwa sala ya adhuhuri. Ama zile mbili za baada husaliwa baada ya sala ya adhuhuri na kabla ya kuingia kwa wakati wa sala ya alasiri. 


Allah ndiye mjuzi zaidi.